Swala ya kwanza ya Ijumaa yafanyika Hagia Sophia Uturuki baada ya kupita miaka 86

Kiswahili Radio 11 views
Swala ya kwanza ya Ijumaa imefanyika leo katika jengo la Hagia Sophia mjini Istanbul baada ya jumba hilo la makumbusho kubadilishwa na kuwa msikiti.

Idadi kubwa ya Waislamu waliwasili eneo hilo tangu mapema leo asubuhi huku maqarii wakisoma Qur'ani tukufu na dua kabla ya kutekelezwa Swala ya Ijumaa adhuhuri ya leo. Rais Recep Tayyip Erdogan alikuwa miongoni mwa mamia ya Waislamu walioshiriki katika Swala hiyo ya kwanza ya Ijumaa katika eneo la kihistoria la Hagia Sophia baada ya kuwa jumba la makumbusho kwa makumi ya miaka.

Swala hiyo ya Ijumaa imefanyika wiki mbili baada ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kutangaza kwamba, jengo hilo lenye umri wa karibu miaka 1,500 litafunguliwa kwa ajili ya ibada ya Waislamu kufuatia uamuzi wa ya Mahakama Kuu wa kubadilishaji matumizi ya jengo hilo lililofanywa jumba la makumbusho na mwanzilishi wa Uturuki ya sasa mwanzoni mwa miaka ya 1930.

Jengo la Hagia Sophia lilitumiwa kama msikiti kwa zaidi ya miaka 481 na likabadilishwa kuwa jumba la makumbusho na mtawala wa zamani wa Uturuki, Mustafa Kemal Ataturk ambaye alipiga vita masuala mengi ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na kubadili hati za Kiatrabu na kupiga marufuku vazi ya staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu, nchini humo. 

Jengo hilo ni miongoni mwa athari muhimu za usanifu majengo katika eneo la Sultan Ahmad mjini Istanbul na lilijengwa katika karne ya 6. 

Add Comments