"Trump! Funga domo lako! Acha kuchochea moto wa ubaguzi! Acha kiu yako ya kumwaga damu"

Kiswahili Radio 10 views
Mkuu wa Kamati ya Habari ya Baraza la Wawakilishi la Marekani ametoa onyo kali kwa rais wa nchi hiyo Donald Trump akimtaka afumbe domo lake, aache kuchochea moto wa ubaguzi wa rangi na kumwaga damu za watu wasio na hatia.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Adam Schiff akitoa onyo hilo kali kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuandika: Sisi ni taifa linalohitajia uadilifu na kuponya majeraha yake, lakini mimi sitaraji kwamba Donald Trump anaweza kulielewa hilo, lakini kwa uchache nategemea kutoka kwake aache kuchochea ubaguzi wa rangi na aachane na kiu yake ya kumwaga damu za watu.

Aidha ameandika: Kama huna uwezo wa kufanya jambo hilo, kwa uchache litendee wema taifa, fumba domo lako!

Siku ya Jumatatu afisa mmoja mzungu wa jeshi la polisi la Marekani alimuua kikatili Mmarekani mmoja mwenye asili ya Afrika katika mji wa Minneapolis, ukatili ambao umezusha wimbi kubwa la maandamano na machafuko katika kona zote za Marekani.

Sasa badala ya rais wa Marekani kutafakari namna ya kutatua tatizo hilo, ametoa vitisho dhidi ya waandamanaji.  Mapema juzi Ijumaa, Donald Trump aliandika ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter na kuwataja waandamanaji wanaolalamikia mauaji ya Mmarekani mweusi kuwa ni magenge ya wahuni na wahalifu. Si hayo tu lakini vile vile alitishia kuwapiga risasi waandamanaji. Aliandika: "Nimewasiliana na Gavana  Tim Walz wa jimbo la Minnesota  na nimemfahamisha kuwa atapata uungaji mkono kamili wa Jeshi na Gadi ya Taifa ya Marekani. Pamoja na matatizo yote yanayojiri, tutaweza kudhibiti hali ya mambo. Iwapo uasi na uporaji wa maduka utaanza, wafanya fujo watafyatuliwa risasi."

Add Comments